Mwaka 2022 mwanamume mmoja huko nchini Chile ambaye alilipwa kimakosa mshahara wake (mara 286 zaidi) aliacha kazi kwenye kampuni hiyo na kutokomea kusikojulikana.
Kwa mujibu wa gazeti la Diario Financiero, Mei 30, 2022, mfanyakazi huyo alifika kwenye ofisi ya meneja wake kuripoti hitilafu iliyotokea katika malipo yake ya mshahara wa kila mwezi.
Baada ya kufuatilia meneja na uongozi wa kampuni hiyo ulithibitisha kwamba mfanyakazi huyo alikuwa amewekewa mamilioni ya pesa kwenye akaunti yake, takriban mara 286 ya mshahara wake kimakosa.
Ofisi ikamwambia mfanyakazi huyo kuwa anapaswa kurudisha pesa hizo mara moja jambo ambalo alikubali na kuahidi angewahi benki mapema siku inayofuata kuzirudishia pesa hizo.
Hata hivyo mfanyakazi huyo hakufanya kama walivyokubaliana bali aliandika barua ya kuacha kazi iliyopelekwa kwenye ofisi hiyo na mwanasheria wake na yeye kutokomea kusikojulikana.