Serikali yalifungia kanisa la Kiboko ya Wachawi

Serikali imeagiza kufungwa Kanisa la Christian Life Church linaloongozwa na Mchungaji Domique Kashoix Dibwe maarufu Kiboko ya Wachawi, lililopo Buza Kwa Lulenge.

 

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kanisa hilo kwenda kinyume cha taratibu za usajili.

 

Barua hiyo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia ya Julai 25, 2024 ambayo Mwananchi imeiona imewaelekeza Mwenyekiti wa Kanisa la Christian Life Church na Mchungaji Dominique Kashoix Dibwe kufunga tawi la Kanisa hilo linaloendeshwa na Mchungaji Dibwe maarufu kwa jina la Kiboko ya Wachawi, lililopo eneo la Buza kwa Lulenge, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

 

Imesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2019, vyenye athari ya kusababisha kanisa hilo kufutiwa usajili wake na kuondolewa kwenye Rejista ya Jumuiya za Kiraia zilizosajiliwa.

 

Miongoni mwa sababu za kufungwa kwake zimetajwa ni kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.

 

Madai mengine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, kutoa mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa lake kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina.

 

Barua hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha imetolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa imesema, madai hayo yanakwenda kinyume cha imani ya Kikristo, Katiba na kanuni za kanisa hilo, ikiwamo kuweka kiwango cha Sh500,000 kwa waumini kupata huduma ya maombezi.

cc MWANANCHI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *