Shakira kutumbuza leo fainali Copa America

Nyota wa muziki kutoka Colombia anayeishi Marekani, Shakira anatarajiwa kuweka rekodi kwa kutumbuiza kwa mara ya kwanza wakati wa mapumziko katika mchezo wa fainali ya Copa America kati ya Argentina na Colombia utakaopigwa kwenye uwanja wa The Hard Rock Stadium, Miami Florida.

 

Mchezo huo ambao utapigwa usiku wa leo kuamkia kesho Jumatatu kwa saa za Afrika ya Mashariki, utamshuhudia mkali huyo wa miondoko ya Pop, mke wa zamani wa Gerard Pique akifanya shoo hiyo kama alivyowahi kufanya kwenye mfululizo wa matamasha ya Super Bowl.

 

Super Bowl michuano ya ligi ya futiboli ya Marekani na imejizolea umaarufu kutokana na matamasha yanayofanywa na wasanii mbalimbali wakati wa mapumziko na Shakira amewahi kutumbuiza, huku pia akitumbuiza kwenye ufunguzi wa Kombe la Dunia mara tatu.

 

Shakira atafanya shoo hiyo ya kipekee katika fainali hiyo ambayo taifa lake la Colombia linacheza.

 

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa mrembo huyu kutumbuiza kwenye uwanja huu kwani alishawahi kufanya hivyo mwaka 2020 akiwa na Jennifer Lopez katika Super Bowl.

 

Mbali na kuimba, Shakira pia ameonyesha ataenda kuisapoti Colombia kwa nguvu zake zote: “Twende Colombia! Tuna timu nzuri, tutaonana Jumapili katika fainali ya Copa America,” aliandika kwenye mitandao yake ya kijamii.

 

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Marekani, katika mashindano hayo nyimbo ya Shakira‘Punteria,’ ndio imekuwa ikipigwa sana na mashabiki ingawa sio wimbo rasmi wa michuano hiyo lakini mashabiki watakuwa wakisubiria kwa hamu kumsikia akiuimba mubashara.

 

Wimbo mwingine kutoka katika albamu yake ya hivi karibuni unaosikilizwa sana ni Las Mujeres Ya No Lloran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *