Tanzania yatoka patupu Olympic 2024 Paris

Rasmi Tanzania imetoka mikono mitupu kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka huu jijini Paris , baada ya Wanariadha wake wawili wa kike wa mbio ndefu Magdalena Shauri na Jackline Sakilu ambao walisalia kama tumaini pekee la Tanzania kuvunja mwiko wa miaka 43 bila Medali ya Olimpiki, kushindwa kutamba leo Jumapili.

Magdalena Shauri amemaliza nafasi ya 40 akitumia muda wa saa 2 dakika 31 na sekunde 58 ambao ndio msimu wake bora, huku Jackline Sakilu akishindwa kabisa kumaliza mbio hizo.

Sifan Hassan Mholanzi mwenye asili ya Ethiopia ndiye ameibuka mshindi akitumia muda wa saa 2:22:55 akiweka rekodi mpya ya Olimpiki na kuvunja rekodi ya Tiki Gelana wa Ethiopia ya muda saa 2:23:07, nafasi ya pili imeenda kwa Assefa Tigst wa Ethiopia akitumia muda wa saa 2:22:58 huku Hellen Obiri wa Kenya akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 2:23:10.

Kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka huu, Tanzania iliwakilishwa na wanamichezo saba (7) wa michezo mitatu, Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu (Riadha), Sophia Latiff na Collins Saliboko (Kuogelea) na Andrew Mlugu (Judo).

Hii ina maana kwamba ni miaka 44 sasa imepita bila ya Tanzania kushinda medali ya Olimpiki, tangu mara ya kwanza na ya mwisho Wanariadha Suleiman Nyambui na Filbert Bayi washinde medali za fedha Olimpiki ya mwaka 1980 jijini Moscow.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *