Mwanajeshi akiri kuiuzia China siri za Jeshi la marekani kwa Milioni 113

Mwanajeshi wa Marekani, Sajenti Korbein Schultz amekiri mashtaka ya kula njama na kuuza siri za jeshi la Marekani kwa China.

Sajenti Korbein alikamatwa mwezi Machi baada ya uchunguzi wa FBI na Jeshi la Marekani kubaini kuwa alilipwa $42,000 (sawa na shilingi Milioni 113 za kibongo) kwa kuuza taarifa nyeti za jeshi hilo.

Sajenti Schultz, ambaye alikuwa na kibali cha kuweza kufikia taarifa nyeti za jeshi la Marekani, alikusanya taarifa zinazohusiana na ulinzi wa makombora na mifumo ya mizinga inayohamishika.

Pia mwanajeshi huyo alikusanya taarifa kuhusu ndege za kivita, mbinu za kijeshi, na mkakati wa ulinzi wa jeshi la Marekani kwa Taiwan.

“Kwa kula njama ili kusambaza taarifa za ulinzi wa taifa kwa mtu anayeishi nje ya Marekani, mshtakiwa huyu aliweka usalama wa taifa letu katika hatari kwa kutumia vibaya imani ambayo jeshi letu iliweka kwake,” alisema Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu, Matthew Olsen wa Kitengo cha Usalama wa Taifa cha Wizara ya Sheria.

Siku ya Jumanne, Sajenti Schultz alikiri mashtaka yote dhidi yake, ikiwa ni pamoja na njama ya kupata na kufichua habari za ulinzi wa taifa na kuchukua hongo kama ofisa wa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *