‘Bundi’ wa majeraha ameendelea kuiandama klabu ya Manchester United baada ya juzi beki wao mpya Leny Yoro kuumia kwenye mchezo wa maandalizi ya msimu dhidi ya Arsenal na kusadikika kuwa nje ya uwanja kwa karibu miezi miwili, leo tena alfajiri washambuliaji wao wawili Marcus Rashford na Antony kuumia na kushindwa kumaliza mchezo kwenye mchezo wa ‘Pre Season’ dhidi ya Real Betis, United wakishinda 3-2.
Kwenye mchezo huo ulichezwa kwenye dimba la Snapdragon Stadium San Diego nchini Marekani, Rashford ambaye alianza alishindwa kuendelea na mchezo kisha kutolewa nje dakika ya 62 baada ya kuumia huku nafasi yake ikichukuliwa na Hanniabal Mejbri.
Pia Antony ambaye aliingia dakika ya 62, alilazimika kutoka nje dakika ya 86 baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Sam Mather.
Magoli ya United kwenye mchezo huo yalifungwa na kiungo wa kati Casemiro, kiungo mshambuliaji Amad Diallo na Rashford huku magoli ya Real Betis yakifungwa na Lloriente na Losada.