Vijana 100 wafungishwa ndoa mbele ya makamu wa Rais Dar

Taasisi ya Kiislamu ya Al Hikmah Foundation imefungisha ndoa vijana 100 wa kiume lengo likiwa ni kuwasaidia kusimama katika maadili na misingi ya dini na kuwasaidia wasio na uwezo wa kulipa mahari wenye nia ya kuoa.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika jana katika Ukumbi wa DYCCC alikuwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Balozi wa Uturuki nchini, Dk Mehmet Gulluoglu na viongozi wa dini wa nchini.

Makamu wa Rais Othman alizungumza kwa uchache na kuwapa nasaha vijana hao waliofungishwa ndoa kuwa msingi wa ndoa upo katika mafunzo na misingi ya dini na si katika mitandao ya kijamii kwani ndoa zinazoendeshwa kwa namna hiyo zimekuwa zikivunjika kila siku.

“Ndoa nyingi zinavunjika kutokana na watu walioko nje ya ndoa hizo, wake, ndugu, dada, kaka wamekuwa wakichochea ndoa nyingi kuvunjika lakini tuwasaidie vijana hawa kuimarisha ndoa hizo,” alisema Othman.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Al Hikma, Shehe Nurdeen Kishki alisema kila mwaka taasisi hiyo inapokuwa inafanya mashindano ya kurani huwa inafanya kitu kuushangaza umma kwa ajili ya kuwasaidia watu.

“Hapo nyuma tulishangaza watu kwa kusaidia wajawazito 100 kwa maana gharama zao za kujifungua tumezibeba sisi pia tukawashangaza tena kwa kuwaozesha watu 70 mwaka jana, mwaka huu katika mashindano ya kurani tulitamka kupeleka watu 10 kwenda hija lakini wamekuwa watu 15 badala ya 10,” alisema Kishki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *