Binti Aliyemkata Koromeo Mtoto Akamatwa

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limefanikiwa kumkamata Clemensia Cosmas Mirembe (19) ambaye anatuhumiwa kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni mtoto Malick Hashim (6) anayeishi eneo la Goba Kinzudi, Kinondoni.

Tukio hilo lilitokea Julai 17, 2024 ambapo binti huyo ambaye alikuwa dada wa kazi alimjeruhi mtoto kisha baada ya tukio mtuhumiwa alikimbia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 22, 2024 na Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema upelelezi wa tukio hilo la kikatili ulianza mara moja na jana Julai 21, 2024 saa 4:00 usiku Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo aliyekuwa mfanyakazi wa nyumba wa ndani aitwaye Clemensia Cosmas Mirembe (19) akiwa amejificha kwenye “pagala” maeneo ya Goba Kizudi Kinondoni.

“Mtuhumiwa huyo anahojiwa kwa kina na atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kwa hatua zaidi za kisheria.

“Wito wetu Jeshi la Polisi ni kuwa pamoja na jitihada ambazo zinaendelea za kuzuia vitendo vya kihalifu tunawashauri wazazi, walezi, walimu, na jamii kwa ujumla kuwafundisha watoto kujenga tabia ya kutembea katika makundi lakini pia watoto wasikubali kuwakaribu na watu wasiowafahamu, watoto wasitumwe maeneo ambayo kwa mazingira ni hatarishi ikiwa ni pamoja na kuacha kuwatuma watoto wadogo maeneo mbalimbali nyakati za usiku,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *