Mume Amtaliki Mkewe Kisa Uzembe Kwenye Maombi

Mahakama moja katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja imevunja ndoa ya miaka minne ya wanandoa baada ya mume kuwasilisha ombi la kutaka ndoa ivunjwe akidai mkewe huwa hamheshimu kwenye ndoa.

Kwa mujibu wa Shirika La Habari La Nigeria, Beshiru Mutairu alielekea mahakamani akitaka ndoa yake ya Kiislamu na mkewe, Amina, kuvunjwa kwa kukosekana kwa upendo na kwamba hazingatii kuswali kwa mujibu wa itikadi za Kiislamu.

Jaji, Mohammed Wakili, alivunja ndoa hiyo Jumanne kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, kufuatia maombi ya Mutairu ya kutaka talaka kwa msingi huo.

Wakili alimuamuru Amina kuanza kuzingatia ‘Iddah,’ ambayo ni muda wa kusubiri unaozingatiwa kwa miezi mitatu kabla ya kufunga ndoa nyingine.

Awali mlalamishi huyo aliiambia mahakama kwamba alifunga ndoa na mlalamikiwa chini ya sheria ya Kiislamu mnamo Machi 17, 2020, na kwamba ndoa hiyo ilibarikiwa na watoto wawili.

Alisema amekuwa na matatizo ya ndoa na mkewe kwa muda mrefu, na kuongeza kuwa hali haijabadilika licha ya familia kuingilia kati.

Kwa hivyo, aliiomba mahakama ivunje ndoa hiyo, akisema hana mapenzi tena naye.

“Haniheshimu kama mume wake na haswali kama Muislamu anavyopaswa,” alisema.

Amina, hata hivyo, alikanusha tuhuma zote dhidi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *